Waombaji wa Mwaka wa Kwanza
Tunapenda
kuwafahamisha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo
2017/2018 kuwa, baada ya uchambuzi wa maombi yao, Orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupangiwa mikopo imekamilika.
Kiasi cha Tshs 34.6 bilioni kimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196. Kwa ujumla, Tshs 108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Orodha
hiyo ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo
(www.heslb.go.tz) na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine (batches)
zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi
zinavyokamilika. Lengo ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata
mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, 2017.
Orodha hii ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua Awamu ya Kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495
waliopata udahili katika chuo kimoja. Itakumbukwa kuwa moja ya sifa kuu
za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika taasisi ya elimu ya
juu inayotambuliwa na Serikali.
Wanafunzi waliopata udahili
katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo,
watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo
watakachojiunga kwa ajili ya masomo.
Tshs 318 bilioni zatengwa kwa ajili ya wanaoendelea na masomo
Wakati huohuo,
tunapenda kuwafahamisha wanafunzi wa elimu ya juu wanaoendelea na
masomo na umma kwa ujumla kuwa tunatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za
mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao
kuanzia leo, Jumatano, Oktoba 18, 2017.
Kiasi cha Tshs 318.6 bilioni kitatolewa kwa wanafunzi 93,295
wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa masomo 2017/2018. Tayari Serikali
imeshatoa fedha hizo na lengo la Bodi ni kuhakikisha fedha zinafika
vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondoloea wanafunzi
usumbufu.
Hitimisho
Bodi ya Mikopo inawasihi waombaji wa
mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha
zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo. Tutaendelea kutoa taarifa
kwa vyombo vya habari na tovuti ya Bodi mara kwa mara.
Kupata orodha kamili
bofya hapa
Mwisho.
Comments